IQNA

Mkenya aibuka mshindi Mashindano ya Kuhifadhi Qur'ani Zanzibar

8:37 - May 29, 2018
Habari ID: 3471536
TEHRAN (IQNA)- Ustadh Twahir Ali Alwi kutoka Kenya ameibuka mashindi wa Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'ani ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo, mashindano hayo yalifanyika Jumapili, Mei 27, 2018, katika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar.

Katibu Mkuu wa Muslim Mercy Youth (MMY) Said Abeid aliyefuatana na Ustadh Twahir Ali Alwi amesema kijana huyo alishinda mashindano hayo mbele ya halaiki ya waumini waliofurika kwenye msikiti wa Jaamiu Zinjibarunaoaminika kuwa ni mkubwa zaidi katika mwambao wa Pwani wa Afrika Mashariki.

Kutokana na ushindi huo, Alwi mwenye umri wa miaka 17 ametunukiwa zawadi ya pesa taslimu TSh4.5 milioni (Ksh225,000) pamoja na cherehani, pasi na zawadi nyingine kadhaa.

Zawadi ya pesa taslimu ni kubwa zaidi kwa miaka 26 tangu mashindano hayo yaanze kufanyika.

Twahir alipata alama za juu kwenye kusoma Qur'ani Tukufu kwa mahadhi na kuhifadhi kitabu kitukufu kizima cha juzuu 30.

Aliwashinda washindani wengine waliotoka mataifa ya Comoro, Uganda, Malawi, Zanzibar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Tanzania Bara na Zanzibar.

Alwi alipata fursa hiyo ya kuwakilisha Kenya kwenye mashindano hayo ya Zanzibar baada ya kushinda mashindano yaliyotayarishwa na MMY yaliyofanyika mwezi uliopita ukumbi wa Tahdhib Muslim School mjini Mombasa.

Abeid alisema kuwa kijana huyo sasa anajitayarisha kwa Mashindano ya Kuhifadhi Qur'ani ya Afrika Mashariki yatakayofanyika viwanja vya Makadara mjini Mombasa siku za Jumamosi na Jumapili hii.

3465966

captcha