IQNA

Raia auawa Sudan katika maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi

22:38 - January 31, 2022
Habari ID: 3474875
TEHRAN (IQNA)- Mtu moja ameuawa jana Sudan wakati maelfu ya wananchi walipoandamana katika mji mkuu Khartoum na miji mingine mikubwa nchini humo kupinga utawala wa kijeshi nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa, waandamanaji, aghalabu wakiwa ni wanawake na vijana, walijitokeza mitaani wakitaka utawala wa kijeshi uondoke madarakni na badala yake serikali ya mpito ya kiraia ichukue usukani nchini humo.

Taarifa zinasema kwa uchache mtu mmoja aliuawa wakati maafisa wa usalama walipojaribu kuwatawanya waandamanaji. 

Takwimu za madaktari zinaonyesha kuwa, hadi sasa watu 74 wamethibitishwa kuuawa na mamia ya wengine wameshajeruhiwa katika maandamano hayo ambayo yalianza Oktoba wakati Jeshi lilipotangaza kutwaa madaraka kikailifu nchini humo.

Licha ya utawala wa kijeshi unaoongozwa na Jenerali Abdul Fattah el Burhan, kuweka sheria kali na kufanya ukandamizaji mkubwa na umwagaji damu, lakini umeshindwa kuzuia wananchi kuandamana. 

Mzozo wa kisiasa nchini Sudan ulipamba moto mwezi Oktoba 15 mwaka jana, kufuatia mapinduzi ya jeshi lililonyakua madaraka ya nchi. Ijapokuwa jeshi la Sudan limejaribu kutafuta njia ya kutatua mzozo uliopo hivi sasa kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya makubaliano na waziri mkuu aliyejiuzulu, Abdallah Hamdok, lakini sera hizo bado hazijafanikiwa. 

Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa, uwepo wa jeshi kwenye madaraka ni kinyume na malengo yao yaliyopelekea kuondolewa madarakani rais wa zamani Omar al-Bashir. Wasudani wanataka kuondoka madarakani kikamilifu jeshi la nchi hiyo na kuanzishwa serikali halali na ya kidemokrasia, lakini maafisa wa jeshi hawako tayari kuondoka madarakani.

Hivi karibuni, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetangaza kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada zake za kupatanisha makundi yote ya kisiasa Sudan ili kutatua mgogoro unaoendelea kutokota nchini humo.

3477624

captcha