IQNA

Qur'ani Inasemaje /12

Utendaji wema kwa mtazamo wa Qur'ani Tukufu

16:43 - June 28, 2022
Habari ID: 3475437
TEHRAN (IQNA) – Vigezo vya utendaji wema vimetajwa katika aya moja ya Qur’ani Tukufu na vinaangazia vyema mtazamo wa Qur’ani Tukufu kuhusu jinsi Waislamu wanavyopaswa kuwa na tabia na imani wanazopaswa kuwa nazo.

Utendaji wema kwa mtazamo wa Qur'ani TukufuAya ya 177 ya Sura Al-Baqarah inaelezea haki na watu wema na kuwasilisha vigezo vya kutenda mema ikiwa ni pamoja na kumwamini Mwenyezi Mungu, Akhera, Malaika na vitabu vya Mwenyezi Mungu pamoja na Infaq (kutoa msaada), kusali, kutoa Zaka ,sadaka, Wafa bil-Ahd (kutimiza ahadi) na kudumisha Taqwa (kumcha Mungu).

Aya hii inasema, “Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao."

Ili kuelewa sehemu ya kwanza ya aya hii, ni vyema  kujifunza maoni ya Sheikh Tabarsi (mwanachuoni wa Kishia wa karne ya 12 Miladia).

Anasema wakati Qibla (eneo ambalo Waislamu wanaelekea wanaposali) kilipobadilika kutoka Al-Quds mjini Quds au Jerusalem hadi Ka’aba Tukufu huko Makkah, mabishano yalizuka kati ya Waislamu, Wayahudi na Wakristo. Wayahudi walisema ingekuwa afadhali kusali kuelekea magharibi ilhali Wakristo walisema sala inapaswa kusemwa wakiwa wametazama mashariki. Aya hii iliteremshwa ili kusisitiza kuwa masuala haya ni ya pembezoni na lililo muhimu ni uadilifu na kutenda mema.

 Kwa mujibu wa aya hii, kuelekea mashariki au magharibi si wema, bali kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu, Akhera, Malaika na vitabu vya Mwenyezi Mungu ni misingi ya amali njema. Uadilifu ni katika kusaidia jamaa, kutoa sadaka kwa mayatima, masikini na wengine wenye mahitaji na kusaidia kuwakomboa watumwa. Mahali pengine katika aya hii, kuswali, kutoa Zaka, kufungamana na ahadi na subira ya mtu katika kukabiliana na magumu pia kunatajwa kuwa ni vigezo vya utendaji amali njema.

Katika tafsiri nyingi za Qur'an, kumekuwa na Hadith kutoka kwa Mtukufu Mtume (SAW) kuhusu aya hii. Mtume (SAW) amesema yeyote atakayeifanyia kazi aya hii, imani yake itakamilika. AlllamAh Tabatabaei mfasiri mashuhuri wa Qur'ani Tukufu, ambaye ameandika tafsiri tajika ya Al Mizan, anaamini kwamba wakati kukifanyia kazi kile ambacho Aya hii inakisema ni kigumu, Aya hii si ya Mitume wa Allah pekee bali pia kwa Maasumin (AS) na Ulil Albab. Ulil Albab ni watu wenye akili, busara hekima, maarifa na utambuzi wa kiwango cha juu.

captcha