IQNA

Iran na jamii ya kimataifa

Rais wa Iran: Sioni faida yoyote ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani

22:14 - September 18, 2022
Habari ID: 3475804
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Iran amesema hana mpango wa kukutana au kufanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani, Joe Biden katika safari yake ya New York, anayotazamiwa kwenda kushiriki Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya CBS News akijibu suali la iwapo yuko tayari kufanya mkutano wa ana kwa ana na Biden.

Akijibu suali hilo aliloulizwa na mtangazaji wa CBS News, Sayyid Raisi amejibu kwa kusema: Hapana, sidhani kama mkutano huo utafanyika. Sidhani mkutano au mazungumzo ya aina hiyo yatakuwa na faida yoyote.

Aidha Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema haoni tofauti yoyote ya kivitendo kati ya serikali ya sasa ya Marekani inayoonozwa na Joe Biden na ya mtangulizi wake Donald Trump, isipokuwa tu katika matamshi.

Ameeleza bayana kuwa, "Wamesema katika jumbe zao kwetu (kwamba wamebadilika), lakini kiuhalisia sisi hatujaona mabadiliko yoyote."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi  Jumatatu ataelekea New York kuhutubia katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu "mfumo wenye haki wa kimataifa kupitia ushirikiano wa kiuchumi wa pande kadhaa."

Akiongoza ujumbe wa ngazi za juu, Raisi atahudhuria mkutano huo wa kila mwaka na kufanya mazungumzo na wakuu wa nchi wanaohudhuria hafla hiyo pamoja na pamoja na viongozi wengine wa taasisi za kimataifa.
Siku ya Jumapili, Rais wa Iran alikutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei aliporejea kutoka mji mkuu wa Uzbekistan wa Samarkand, ambako alihudhuria mkutano wa 22 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO).
Raeisi aliwasilisha ripoti kuhusu ziara yake ya Uzbekistan na kumfahamisha Ayatullah Khamenei kuhusu safari yake ijayo ya UNGA.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa kwake na ripoti hiyo na hatua zilizochukuliwa na kumtakia mafanikio mema rais huyo katika mkesha wa safari yake ya mjini New York.

4086319

captcha