IQNA

Wananchi wa Iraq waungana na jeshi kupambana na magaidi wa Daesh

20:20 - June 13, 2014
Habari ID: 1417080
Harakati za kundi la kigaidi la DAESH katika maeneo mbalimbali ya Iraq zimekuwa sababu ya mshikamano na umoja kati ya makundi mbalimbali ya taifa la nchi hiyo.

Makundi mbalimbali ya wananchi wa Iraq ambayo yametambua hali nyeti ya kipindi cha sasa yameunga mkono operesheni kali inayofanywa na jeshi la nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya kundi hilo la kitakfiri na kiwahabi na kuanza kujiunga na vikosi vya jeshi kwa ajili ya kulinda ardhi na matukufu yao ya kidini.

Vyombo vya habari ndani ya Iraq vinaripoti kuwa maelfu ya raia katika mkoa wa Babel wamejiunga na jeshi la nchi hiyo katika mikoa ya Nineveh, Salahuddin na Kirkuk. Vilevile kumeripotiwa habari za kujiandikisha maelfu ya raia wa Iraq katika mikoa mingine ya nchi hiyo kwa ajili ya kujiunga na operesheni ya jeshi ya kukabiliana na magaidi wa kundi la DAESH. Mjini Basra peke yake raia elfu 13 wametangaza kwamba wako tayari kujiunga na jeshi katika operesheni ya kuliangamiza kundi hilo la kigaidi.  Raia elfu saba pia kutoka mkoa wa Wasit wamejiunga na jeshi katika siku tatu zilizopita.

Makundi ya Ahlusunna, Wakurdi na hata wapiganaji wa kundi la Pishmarg pia wamejiunga na jeshi la Iraq kwa ajili ya kulinda ardhi na matukufu ya nchi hiyo.

Habari zinasema kuwa kutokana na wimbi hilo la wananchi za kusaidiana na jeshi, wapiganaji wa kundi la kigaidi la DAESH wamelazimika kurudi nyuma na kuondoka katika baadhi ya maeneo ya Mosul na Kirkuk.

Kwa sasa mji wa Samurra ambao una Haram mbili za wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) unalindwa vikali kwa kuchelea mashambulizi ya kundi hilo la kiwahabi ambalo limekuwa likivunjia heshima makaburi ya watu watukufu na masahaba wa Mtume. Idadi kubwa ya watu wanaolinda mji huo ni raia wa kawaida waliojitolea kupambana na magaidi.

Nukta nyingine muhimu katika hali ya sasa ya Iraq ni mchango wa viongozi wa dini katika kuwahamasisha wananchi na kuhimiza umoja na mashikamano na jeshi la nchi hiyo. Kwa mfano tu kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi wa kidini nchini humo Ayatullah Ali Sistani amewataka Wairaqi kujiepusha na mifarakano katika kipindi hiki muhimu na kufanya juhudi za kulinda nchi yao. Maulamaa na wanazuoni wa madhehebu ya Suni pia wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono mapambano ya jeshi na wananchi dhidi ya kundi hilo la kigaidi ambalo shari yake haitofautishi baina ya Shia na Suni.

Vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya kidini na kikaumu ya Iraq yanasisitiza juu ya udharura wa kulinda nchi, na kutilia mkazo kwamba umoja na mshikamano wa kitaifa ndiyo siri ya ushindi mbele ya fitina ya magaidi wa kundi la DAESH.

Licha ya kwamba Iraq inakabiliwa na hatari kubwa katika kipindi cha sasa lakini mshikamano wa wananchi na kuungana kwao na jeshi vimeonesha kuwa Wairaqi wote wako tayari kujitolea mhanga kwa ajili ya kulinda matukufu na maslahi yao ya kitaifa licha ya hitilafu zao za ndani.

1417040

Kishikizo: iraq daesh magaidi
captcha