IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran itakabiliana vilivyo uchokozi dhidi yake

18:17 - April 20, 2015
Habari ID: 3180160
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haijawahi kuwa tishio kwa usalama wa eneo la Mashariki ya Kati na nchi majirani zake na katika siku za usoni pia haitokuwa hivyo, lakini wakati huo huo itaendelea kusimama kidete kukabiliana vilivyo na uchokozi wa aina yoyote ile dhidi yake.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo jana Jumapili wakati alipoonana na makamanda, maafisa na familia za mashahidi wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na huku akiashiria namna majeshi mengi duniani yasivyoheshimu sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu wakati majeshi hayo yanapopata ushindi fulani na kusisitiza kuwa: Mfano wa wazi wa suala hilo ni mambo yanayotendwa na madola ya kibeberu duniani hususan Marekani ambayo hayajali sheria zozote za kimataifa wala misingi ya kibinadamu, na yanafanya kila aina ya jinai dhidi ya mataifa mengine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja matukio ya Yemen, vita vya Ghaza na vita vya Lebanon kuwa ni mifano mingine ya kutoheshimu madola hayo na sheria za kimataifa na kusisitiza kuwa: Vikosi vya ulinzi vya Iran daima vimekuwa vikiheshimu sheria za kimataifa na kamwe havikanyagi sheria iwe ni wakati wa kupata ushindi au wakati wa hatari na wala haitumii silaha zilizopigwa marufuku wala mbinu zisizo sahihi.
Vile vile amegusia ngano za uongo zinazoenezwa na Wamarekani, madola ya Ulaya na baadhi ya vibaraka wao za kwamba eti Iran ina mpango wa kumiliki silaha za nyuklia ikiwa ni njama za madola hayo za kuionesha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni tishio kwa usalama wa dunia na kuongeza kuwa, tishio kubwa la usalama wa dunia na eneo la Mashariki ya Kati ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel madola ambayo hayajali misingi yoyote ya kidini na kibinadamu na yanavamia popote pale yanapoamua na kufanya mauaji kwa kinyama kwa kiasi chochote yanachotaka.../EM

3172363

captcha