Nusaiba Mubarak, 26, alikuwa anasubiri kutoa ushahidi kuhusu ukatili wa maafisa wa LAPD, wakati maafisa watatu wa polisi walipomuhujumu ghafla, kumuweka pingu na kumuingiza katika chumba kingine ambapo walimvua mtandio wake na kumdhalilisha.
Mubarak ambaye anawakilishwa na mawakili wa Baraza la Marekani la Mahusiano ya Kiislamu (CAIR), amesema kitendo cha maafisa wanaume kumvua Hijabu hni ukiukwaji wa mafundisho ya Kiislamu. Aidha amesema kukamatwa kwake kulikuwa kinyume cha sharia kwani hakuwa amefanya kosa lolote. Aidha anasema aliachiliwa pasina kufunguliwa mashtaka na kuongeza kuwa tukio hilo lilimshtua sana.
Bi. Mubarak anasema alikuwa amehudhuria kikao cha Tume ya Polisi Septemba mwaka jana kulaani mauaji ya Albert Ramon Dorse, ambayo alipigwa risasi na kuuawa na afisa wa LAPD mnamo Oktoba 2018. Baada ya kukamatwa na kuvuliwa Hijabu, Bi. Mubarak hakuweza kutoa ushahidi katika tume hiyo.