IQNA

Sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zaanza rasmi Iran

16:24 - February 01, 2022
Habari ID: 3474878
TEHRAN (IQNA) – Sherehe za mwaka wa 43 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 zimeanza rasmi kote Iran.

Sherehe hizo zimeanza kwa hafla iliyofanyika katika Haram ya Imam Khomeini MA, hayati muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hafla ya leo imeanza kwa qiraa ya Qur'ani Tukufu ya qarii mashuhuri Ustadh Habib Sedaqat na kufuatiwa na wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baada ya hapo Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran alitoa hotuba ambapo amemtaja Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu-kuwa ni mwanazuoni aliyeinukia katika chuo cha Qur'ani Tukufu.

Ikumbukwe kuwa, Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

4032846

 

 

captcha