IQNA

Hali ya Afghanistan

Nchi za Kiislamu zalaani Taliban kuwazuia wanawake Afghanistan kusoma vyuo vikuu

21:12 - December 23, 2022
Habari ID: 3476291
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) imebainisha masikitiko yake kuhusu uamuzi wa utawala wa Taliban nchini Afghanistan kuwapiga marufuku wanawake kuendelea na elimu katika vyuo vikuu nchini humo.

OIC imesema katika taarifa yake kwamba Katibu Mkuu wa jumuiya Hissein Brahim Taha analaani hatua hiyo.

Katibu mkuu na mjumbe wake maalum walikuwa wameonya dhidi ya uamuzi huo mara kadhaa hapo awali, ikiwa ni pamoja na wakati wa ziara ya mjumbe huyo mjini Kabul mwezi Novemba, taarifa hiyo iliongeza.

Brahim Taha alisema kusimamishwa kwa wanafunzi wa kike kupata masomo katika vyuo vikuu kunadhoofisha haki ya kijamii na kunadhuru pakubwa itibari na hadhi ya Taliban.

OIC ilitoa wito kwa Taliban kufikiria upya uamuzi huo kulingana na ahadi za hapo awali zilizotolewa na kundi hilo lenye itikadi za Kiwahhabi ambalo linatawala Afghanistan hivi sasa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric pia amelaani hatua hiyo, akiielezea kuwa "inayokera".

Siku ya Jumanne, wizara ya elimu ya juu ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan ilisema kuwa wanafunzi wa kike hawataruhusiwa kuingia katika vyuo vikuu vya nchi hiyo hadi ilani nyingine.

Kimsingi hatua hii ingepiga marufuku elimu ya wanawake nchini Afghanistan.

4108891

captcha