IQNA

Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Waislamu wanataraji hatua za kivitendo kukabiliana na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

14:22 - April 20, 2023
Habari ID: 3476894
TEHRAN (IQNA)- Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, haitoshi kulaani tu hujuma za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa na mashambulio dhidi ya wauminii wa Kipalestina walioko katika hali ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Rais Ibrahim Raisi alisema hayo jana katika dhifa ya futari na mabalozi wa nchi za Kiislamu walioko hapa Iran ambapo sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa kukaribia maadhimisho ya sikukuu ya Idul-Fitr amesisitiza kuwa, haitoshi tu kulaani na kuonyesha kuchukizwa na jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, hii leo Waislamu wanataraji kuona kukichukuliwa hatua za kivitendo kwa ajili ya kukabiliana na jinai za utawala ghasibu wa Israel sambamba na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Aidha amesema, utatuzi wa kadhia ya Palestina ni ule ubunifu na pendekezo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei la kuainishwa mustakabali wa Palestina na kuundwa serikali inayotakiwa na Wapalestina kupitia kura za Wapalestina.

Kadhalika Sayyid Ibrahim Raisi amesema, kuzusha mifarakano, kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri, kufanya hujuma na uvamizii na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu ni miongoni mwa mipango michafu ya adui inayolenga kudhoofisha jamii za Kiislamu.

Vilevile Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, ili kukabiliana na njama hizo za maadui, mataifa ya Kiiislamu hayana budi kudumisha umoja na mshikamano baina yao.

captcha