IQNA

Jinai za Israel

Wataalamu wa Kisheria: Shambulio la Kijeshi la Israel dhidi ya Jenin ni Uhalifu wa Kivita

17:23 - July 15, 2023
Habari ID: 3477286
AL-QUDS (IQNA) – Wataalamu wa sheria wamebaini kuwa sheria za Mkataba wa Geneva kuhusu uhalifu wa kivita zilikiukwa katika shambulio la mauaji la jeshi la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin katika sehemu ya kaskazini ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Susan Akram, mhadhiri katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Boston, alisema uvamizi huo, ambao uliua Wapalestina 12 na kujeruhi makumi ya wengine, ni sawa na uhalifu wa kivita kwa sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kushambulia kwa makusudi raia wengi na kushambulia vitengo vya matibabu.

"Makubaliano ya Geneva yanahusi uhalifu wa kivita wakati wa uvamizi, mauaji ya kukusudia, kusababisha mateso makubwa kwa makusudi kwa watu ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na uharibifu mkubwa wa mali usio na ulazima wa kijeshi," Akram alisema wakati wa mkutano wa wavuti ulioandaliwa mapema wiki hii na Kituo cha Kiarabu Washington, DC. .

Ameongeza kuwa hakuna shaka kwamba kile Israel ilifanya huko Jenin ni uhalifu wa kivita.

Daniel Levy wa Mradi wa Marekani/Mashariki ya Kati na mwandishi wa habari Dalia Hatuqa, wanajopo wengine kwenye mtandao huo, pia walikubaliana kwamba hatua za Israel katika Ukingo wa Magharibi ni sawa na uhalifu wa kivita.

Akram alisema propaganda iliyotumiwa na Israel kwamba uvamizi wa Jenin na miji mingine ya Palestina kama Nablus ni jaribio la kung'oa makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina haizuii matendo yake kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa.

Akiashiria kwamba Ukingo wa Magharibi ni eneo linalokaliwa kwa mabavu, alisema, "mashambulizi ya Israel dhidi ya wakazi ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu  ni uhalifu kwa sababu sheria ya uvamizi inakataza wavamizi kutumia mashambulizi ya kijeshi dhidi ya maeneo ya kiraia katika eneo linalokaliwa kwa mabavu."

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), nyumba 900 za Wapalestina ziliharibiwa na nyingi kati ya hizo haziwezi kukaliwa na watu baada ya jeshi la Israel kuvamia kambi ya wakimbizi ya Jenin hivi karibuni.

Adnan Abu Hasna, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa, alisema Jumanne kwamba wenzake bado wanaandika ripoti kuhusu uharibifu uliotokea ndani ya kambi wakati wa mashambulizi.

Kipaumbele cha UNRWA ni kusaidia kurejesha hali ya kawaida kwa kurejesha huduma zake kama vile elimu, huduma za afya na usafi wa mazingira, aliongeza.

Wiki iliyopita, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilisema mashambulizi ya kijeshi ya Israel yaliyolenga kambi ya wakimbizi ya Jenin "huenda ikawa uhalifu wa kivita."

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa walibaini kuwa, "operesheni za jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kuua na kujeruhi vibaya Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na Israel, kuharibu makazi na miundombinu yao, na kuwahamisha maelfu kiholela, ni sawa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na viwango vya kimataifa vya matumizi ya nguvu na inaweza kuwa uhalifu wa kivita."

3484342

Habari zinazohusiana
Kishikizo: jenin jinai za israel
captcha