IQNA

Njia ya Ustawi / 3

Qur'ani Tukufu; Kitabu cha Mwongozo, Ufahamu

19:07 - December 05, 2023
Habari ID: 3477990
TEHRAN (IQNA) – Qur’ani Tukufu imetambulishwa kama kitabu cha mwongozo, nuru, uponyaji, rehema, ukumbusho, na utambuzi na ambacho kinatoa mpango sahihi wa maisha.

Kwa kutenda kulingana na mafundisho ya kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu, wanadamu wanaweza kupata wokovu wa milele.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 57 ya Sura Yunus: “ Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini".

Allamah Tabatabai anasema ikiwa sifa nne zilizotajwa katika aya hii ya Qur'ani Tukufu zinalinganishwa na Qur'ani yenyewe, basi tunaweza kusema aya hii inatoa muhtasari wa kina wa uzuri na usafi wa Kitabu Kitukufu.

Kwa hakika, aya hii inaangazia hatua nne za ukuaji wa mwanadamu na kuelekea kwenye ukamilifu kama matokeo ya kufuata mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

  1. Ushauri na Mawaidha
  2. Kuisafisha nafsi na maovu yote ya kimaadili
  3. Mwongozo, unaofanyika baada ya utakaso, ambao unamaanisha kuelekea kwenye ukamilifu katika nyanja zote chanya.
  4. Kumsaidia mwanadamu kustahiki kupata rehema na baraka za Mungu.

Hatua hizi huja moja baada ya nyingine na zote hufikiwa kutokana na kuyafanyia kazi mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

Kwa hakika, Qur'ani Tukufu inatoa nasaha kwa watu, inazisafisha nyoyo na dhambi na maovu, na kuwapa nuru ya uongofu. Na ni Qur'ani Tukufu inayoleta baraka za Mwenyezi Mungu kwa watu binafsi na jamii.

Imam Ali (AS) amesema: “Kwa hiyo, tafuta tiba kutoka kwayo (Qur’ani Tukufu) kwa maradhi yako na utafute msaada katika dhiki zako. Ina tiba ya magonjwa makubwa zaidi, yaani kutoamini, unafiki, uasi na upotofu.”

captcha