IQNA

Mrengo wa Muqawam

Nasrallah: Jibu la Iran kwa hujuma ya Israel ni haki ya kisheria

17:39 - April 09, 2024
Habari ID: 3478656
IQNA- Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah amesema, haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutoa jibu kwa uchokozi uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa kushambulia ubalozi wake mdogo mjini Damascus ni haki yenye uhalali wa kisheria.

Nasrallah aliyasema hayo jana Jumatatu, katika hafla ya kuwakumbuka mashahidi wa shambulio la kigaidi lililofanywa na utawala wa Kizayuni lililolenga ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria, iliyofanyika katika ukumbi wa Majmau-Sayyidi-Shuhadaa ulioko kwenye vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut na akabainisha kuwa, nchi zote duniani zimekiri kwamba Iran itatoa jibu kwa hujuma ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni, na kusisitiza kuwa jibu la Iran kwa uchokozi huo ni haki ya kimaumbile na yenye uhalali wa kisheria.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, kulengwa washauri wa Kiiran katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ni uvamizi na uchokozi mkubwa zaidi kufanywa na Israel nchini Syria katika miaka ya hivi karibuni, na akabainisha kuwa kuwalenga washauri wa Kiiran nchini Syria ni sehemu ya vita kuu vya adui Mzayuni.

Nasrallah ameongeza kuwa, baada ya kupita zaidi ya miezi sita tangu vilipoanza vita dhidi ya Ghaza vya utawala wa Israel mfanya mauaji ya kimbari, malengo ya adui yaliyotangazwa hayajafikiwa na hali ya Israel imekuwa mbaya zaidi kwa kila namna.

Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, na kimya cha Jamii ya Kimataifa na taasisi za haki za binadamu kuhusiana na jinai za Israel zimepelekea kuendelea mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na utawala huo haramu.

3487873

captcha