IQNA

Rais Raisi: Kuondoka Marekani Afghanistan ni fursa ya kufufua maisha, amani

20:39 - August 16, 2021
Habari ID: 3474197
TEHRAN (IQNA) -Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran amesema kushindwa kijeshi na kuondoka Marekani Afghanistan inapasa kuwe ni fursa ya kufufua maisha, amani na usalama endelevu ndani ya nchi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika mazungumzo na waziri wa mambo ya nje Mohammad Javad Zarif na akaeleza kwamba, usalama, uthabiti na ustawi wa jamii ni haki ya watu wa Afghanistan. 

Aidha amesema Iran itafanya jitihada kurejesha utulivu na uthabiti nchini Afghanistan ambalo ndilo hitajio la kwanza la nchi hiyo kwa sasa.

Amesisitiza kuwa, Iran itafanya jitihada kwa ajili ya kurejesha uthabiti nchini Afghanistan ambalo ni hitajio la kwanza la nchi hiyo hivi sasa; na kutokana na kuwa nchi ndugu na jirani wa Afghanistan inatoa mwito kwa makundi yote kutafuta mwafaka wa kitaifa.

Seyyid Raisi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, kutawala irada na matakwa ya wananchi wa Afghanistan ndiko siku zote kunakowezesha kupatikana amani na uthabiti nchini humo na akasisitiza kuwa, Iran inafuatilia kwa makini matukio ya Afghanistan na itaendelea kuheshimu uhusiano wa kiujirani uliopo baina yake na nchi hiyo.

Baada ya kuitoroka nchi jana Jumapili, Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan alituma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema, ameihama nchi ili kuepusha uharibifu, umwagaji damu na maafa makubwa ya kibinadamu.

Jana hiyo hiyo, kundi la Taliban lilidhibiti Ikulu ya Rais katika mji mkuu Kabul na kusisitiza kuwa litahakikisha amani inarejea mjini humo na katika miji mingine ya Afghanistan.

3991146

Kishikizo: raisi iran afghanistan
captcha