IQNA

Baraza la Usalama la UN lakutana kujadili mgogoro wa Afghanistan

12:11 - August 17, 2021
Habari ID: 3474198
TEHRAN (IQNA)-Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana Jumatatu kwa dharura kujadili hali nchini Afghanistan ambako kundi la Taliban llilichukua mamlaka Jumapili baada ya vikosi vya serikali kuzidiwa nguvu na Rais ashraf Ghani kutoroka nchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa,  "ulimwengu unafuatilia kinachoendelea huko Afghanistan kwa moyo mzito na wasiwasi mkubwa  hasa kuhusu yatakayofuata."

Aidha amehimiza pande zote husika katika mgogoro wa Afghanistan, haswa  kundi laTaliban, kujizuia kabisa ili kulinda maisha na kuhakikisha kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaweza kutimizwa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kwamba mzozo huo ulikuwa umelazimisha mamia ya maelfu ya watu kuondoka majumbani mwao na kwamba Kabul imeshuhudia idadi mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao. 

Guterres amezikumbusha pande zote katika mzozo juu ya wajibu wao wa kulinda raia na kuwataka wayape mashirika ya kibinadamu fursa ya kufika bila vizuizi ili kutoa huduma na msaada haraka kwa wanaouhitaji.

Pia amezitaka nchi zote kukubali kupokea wakimbizi wa Afghanistan na kujiepusha na kuwafukuza.  

Baraza la Usalama limetaka mapigano yasitishwe mara moja nchini Afghansitan na pande zote hasimu zifanye mazungumzo.  

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa akizungumza aktika kikao hicho amebainisha wasiwasi kuhusu kushadidi mapigano Afghanistan. Ameongeza kuwa Moscow inaamini kuwa, Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika  hali ya hivi sasa inayoshuhudiwa Afghanistan.

Marekani ilivamia Afghanistan mnamo Oktoba 2001 na kuwaondoa Taliban madarakani. Vikosi vya Marekani vimeikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa takriban miaka 20 kwa kisingizio cha kuangamiza kundi la Taliban. Lakini baada ya wanajeshi wa Marekani na waitifaki wake kuondoka Afghanistan hivi karibuni,  kundi la Taliban limeibuka tena kwa nguvu zake zote na sasa linapanga kuteka na kuudhibiti mji mkuu, Kabul.

3991249

captcha