IQNA

Pakistan yaandaa mkutano wa OIC kuhusu Afghanistan

17:20 - December 18, 2021
Habari ID: 3474692
TEHRAN (IQNA) Jumapilia 19 Disemba, mji mkuu wa Pakistan, Islamabad utakuwa mwenyeji wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambapo jenda kuu na pekee ya mkutano huo ni kuchunguza matukio ya Afghanistan hususan hali ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Shah Mehmood Qureshi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan amefafanua kuhusu mkutano huo na kusema kwamba: " kuwa: Tumeazimia kuunda kambi ya pamoja kwa ajili ya kuisaidia Afghanistan na wakati huo huo tuko macho na aina yoyote ile ya matokeo mabaya ya kushtadi mgogoro wa nchi hiyo na matokeo yake kwa mataifa jirani, ya kieneo na ulimwengu kwa ujumla."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan amezungumzia kuzidi kuongezeka uwezekano wa kusambaratika kabisa muundo wa kimaisha na kiuchumi wa Afghanistan na kueleza kwamba, kama hakutachukuliwa hatua za haraka za kuzuia hilo, basi eneo lote la Asia Magharibi hususan mataifa jirani na  chi hiyo yatakumbwa na matokeo mabaya ya hilo.

Mpango uliotangazwa wa Pakistan wa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa ajili ya kuchunguza na kutathmini matukio ya Afghanistan na kuchukuliwa hatua za lazima kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo unatathminiwa na weledi wa mambo kuwa ni katika fremu ya sera za Islamabad za kudumisha utawala wa Taliban nchini Afghanistan.

Tangu wanamgambo wa Taliban waliposhika tena hatamu za uongozi nchini Afghanistan Agosti 15 mwaka huu (2021), Pakistan ndio nchi pekee ambayo imetoa himaya kubwa zaidi ya kisiasa kwa kundi hilo katika eneo na katika uga wa kimataifa. Mkakati muhimu zaidi kwa sasa wa Pakistan kuhusiana na kuliunga mkono kundi la wanamgambo wa Taliban ni kusaidia kuzikinaisha nchi na asasi mbalimbali za kimataifa ili ziutambue rasmi utawala wa kundi hilo. Pakistan ikiwa na nia ya kuhakikisha lengo hilo linafikiwa imejikita zaidi kwa mataifa ya Magharibi hususan Marekani.

Kwa mtazamo wa viongozi wa ngazi za juu wa Pakistan ni kuwa, kama nchi hiyo itaweza kuikinaisha Marekani iitambue serikali ya Taliban nchini Afghanistan, sehemu kubwa ya matatizo na vizingiti vya kisiasa vya kundi hilo vitaondolewa kama ambavyo matatizo ya kifedha ya serikali ya Taliban yatapungua kwa kuachiliwa fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa na serikali ya Washington.

Hasa kwa kutilia maanani kwamba, chama tawala nchini Pakistan cha Tahreek-e-Insaf kinaamini kuwa, kama Marekani itaitambua rasmi serikali ya Taliban kutafunguliwa njia ya kutumia mbinu kama hiyo kwa mataifa mengine hasa ya Kiarabu.

Hata hivyo kuna matazamo huu baina ya viongozi wa Pakistan hususan Waziri Mkuu Imran Khan kwamba: Kuna sababu mbalimbali ambazo zitaifanya Marekani ilazimike kuitambua serikali ya Taliban nchini Afghanistan.

Katika mazingira kama haya, hatua ya Pakistan ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya KIgeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inafuatilia kuhakikisha kwamba, katika hatua ya kwanza mataifa hayo yanasaidia Afghanistan iondokane na changamoto ya kiuchumi na katika itakayofuata iandae mazingira ya kutambuliwa rasmi utawala wa Taliban na nchi wanachama wa jumuiya ya OIC.

Pakistan inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu {OIC} katika hali ambayo, hivi karibuni kundi la Taliban liilitaka jumuiya hiyo kuutambua rasmi utawala wake nchini Afghanistan. Ukweli wa mambo ni kuwa, mataifa ya Kiislamu nayo kama ilivyo jamii ya kimataifa yana kigugumizi kikubwa katika kuitambua rasmi serikali ya Taliban nchini Afghanistan.

Wasiwasi wa mataifa ya Kiislamu ni kuwa, wanamgambo wa Taliban wanatumia madai ya kuanzisha utawala wa Kiislamu nchini Afghanistan ambapo sambamba na kupuuza haki za makundi na kaumu nyingine nchini humo kwa namna fulani wamehodhi madaraka peke yao kupitia ukandamizaji na kuwatwisha mambo watu suala ambalo linakinzana wazi kabisa na mafundisho ya Uislamu ambayo yanakokoteza na kutilia mkazo suala la kuheshimiwa haki za kila mtu.

3476976

captcha