IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu /69

Sura Al-Haqqah; Uhakika wa Siku ya Kiyama

20:47 - April 03, 2023
Habari ID: 3476806
TEHRAN (IQNA) – Al-Haqqah ni miongoni mwa majina ya Siku ya Hukumu au Siku ya Kiyama. Inamaanisha kitu ambacho ni hakika, kilichoamuliwa na chenye uhakika. Sura inawaonya wale wanaoikadhibisha Siku ya Kiyama na inaonesha hali yao siku hiyo.

Al-Haqqah ni jina la sura ya 69 ya Qur'ani Tukufu yenye aya 52 na iko katika Juzuu ya 29. Ni Sura ya 78 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Katika aya tatu za mwanzo neno Al-Haqqah limerudiwa na hivyo jina la Sura limetokana na neno hilo.

Al-Haqqah maana yake ni jambo ambalo ni la hakika, lililodhamiriwa na la kweli na sababu ya kuirudia Sura ni kutoa onyo kuhusu Siku ya Kiyama.

Dhamira kuu ya Sura hii ni Siku ya Hukumu na maelezo yake. Inazungumza juu ya ukweli kwamba hakika itakuja na juu ya hatima ya wale wanaoikana.

Sura hiyo ina sehemu kuu tatu. Ya kwanza ni kuhusu yale yaliyowapata watu walioishi zamani. Watu kama wa kina Adi, Thamud, Lut'i na Firauni waliokataa mwito wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakapata adhabu ya Mwenyezi Mungu. Pia inazungumza juu ya kile kilichotokea kwa wale waliomwamini Nuhu (AS) na kuokolewa kwa kuingia kwenye Safina ya Nuhu.

Sehemu ya pili inafafanua Siku ya Kiyama na jinsi watu wanavyogawanyika siku hiyo. Kutakuwa na makundi mawili ya watu: Wale walio pewa kitabu chao kwa mkono wao wa kulia. Hao ndio wanaofurahi siku hiyo.

Na wapo walio pewa kitabu chao kwa mkono wao wa kushoto. Wanahuzunika na wanangoja adhabu kali kwa yale waliyoyafanya hapa duniani.

Sehemu ya tatu ya Sura inajumuisha msisitizo mkubwa juu ya ukweli wa Quran na utume na mjumbe wa mwisho wa Mungu. Pia kuna msisitizo juu ya ukweli kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kamwe hazushi dhidi ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa aya za mwisho za Sura, ikiwa mtu anadai kwa uwongo kuwa nabii wa Mungu, hata kama watu watashindwa kuutambua uwongo wake, hakika Mungu atafichua uwongo wake na kumwadhibu.

captcha